Friday, 23 September 2016

ALICHOKIANDIKA ZITO KUHUSU ESCROW

Rais Magufuli aonyeshe hasira zake dhidi ya Ufisadi kwenye huu ufisadi mkongwe wa IPTL.


Nimesoma "Arbitral Award" (Hukumu ya Kesi) ambayo Benki ya Standard chartered wametunukiwa na ICSID (Kesi Na. ARB/10/20) na Kwa Kweli nimeumizwa sana na nilichokikuta.

Ukweli ni Kwamba hoja zote ambazo zimetumika kuwapa ushindi SCB ndizo Kamati ya Bunge ya Mahesabu ya Mashirika ya Umma (PAC) ilizijenga kwenye Taarifa yake Maalumu iliyopitishwa na Bunge na kutolewa maazimio 8.

Ndio hoja hizo hizo zilibezwa na Serikali ya CCM na Umma kuaminishwa kuwa Fedha Husika zimelipwa Kwa Watu Sahihi Na Kwamba TANESCO hawatakuwa na madai dhidi Yao mbeleni. Kinyume Kabisa Na hali ilivyo sasa.

Mahakama hii (Tribunal) ya ICSID imethibitisha maonyo ya Kamati ya PAC kwamba hasara Kwa Nchi kwenye kashfa ya #TegetaEscrow itakuwa ni mara mbili ya Fedha zilizochotwa kwani mwenye Mali akijulikana tutapaswa kumlipa tena.

• Tulimpa Harbinder Singh Seth wa Kampuni ya Kitapeli ya PAP Shilingi za Kitanzania Bilioni 306 bilioni.

• Sasa tunapaswa kuwalipa Standard Chartered Bank (Hongkong) Ltd Shilingi za Kitanzania Bilioni 320.

• Jumla tutakuwa tumelipa pasipo Sababu Kabisa Shilingi za Kitanzania Bilioni 626. Fedha Hizi Ni zaidi ya Mara 6 ya Bajeti ya Maendeleo ya Wizara ya Kilimo. Fedha Nyingi Kiasi hiki zingeweza kabisa kusaidia Maendeleo ya Kilimo Na kuinua Maisha ya zaidi ya 65% ya Watanzania Wote.

• Fedha Hizi Ni zaidi ya Mishahara ya Wafanyakazi Wote wa Serikali Kwa Mwezi Nchi Nzima. Takwimu za Mwezi Juni Mwaka huu zinaonyesha Jumla ya Mishahara ya wafanyakazi Wote wa Serikali Nchi Nzima Ni Shilingi Bilioni 570. Hela Hizi Za Kifisadi za Escrow zinakwenda kuwafaidisha Matapeli wachache Tu - Inauma Mno.

• Baada ya Hukumu hii si tu tatalipa Bilioni 626, Lakini bado tunamlipa Seth kila Mwezi Dola Milioni 4 (Sawa na zaidi ya Bilioni 8.7 za Kitanzania) Kwa umeme wa mtambo uliomilikishwa Kifisadi Kwa Kampuni ya Kitapeli.

MUHIMU: Rais John Magufuli ana fursa ya kihistoria kumaliza kabisa huu mtandao wa wizi na utapeli uliodumu toka mwaka 1995. Watanzania Masikini na Wanyonge tutakuwa Nyuma yake kwenye hili. Atende Sasa.

Zitto Kabwe Ruyagwa
Sept 21, 2016

No comments:

Post a Comment