Simu ya kisasa ya Samsung Galaxy S7 inayopigiwa upatu kuwa na uwezo wa kustahimili kuwa chini ya maji imefeli majaribio ya shirika la moja la kutathmini ubora wa bidhaa za kielektroniki. Programu ya simu hiyo ya Samsung Active ilizima punde baada ya kutumbukizwa ndani ya pipa la maji. Kampuni hiyo ya kutathmini ubora wa bidhaa, Consumer Reports ilirejelea jaribio hilo kwa mara ya pili wakitumia simu tofauti na kama ile ya kwanza ikafeli. Kampuni ya kutengeza simu hiyo ya Samsung ikijitetea imesema huenda simu hizo zilikuwa ni mbovu na hivyo kuruhusu maji kuingia ndani. Simu hizo zilitumbukizwa ndani ya mapipa ya maji na kutolewa baada ya dakika. Simu hizo za Samsung zilizima. Kulikuwa hata na maji katika eneo la kamera za simu hizo mbali na viputo. Kampuni inayotengeza simu hizo kutoka Korea Kusini Samsung imejitetea vikali ikisema kuwa Galaxy S7 Active, inayouzwa Marekani imefanyiwa majaribio kabambe na hata kupewa cheti maalum cha IP68.