Friday, 27 October 2023

MGOGORO WA ISRAEL NA PALESTINA-3

 

HAMAS: KUTOKA KIKUNDI CHA KUTOA MISAADA MPAKA KIKUNDI CHA KISIASA NA KIJESHI.

                                 Jeshi la Israel 

Ili kuelewa imani na itikadi kali ya Hamas kabla hata kuundwa kwake tuone kidogo ikitikadi ya Waarabu juu ya taifa la Israel hasa kabla ya vita vya siku sita [5-11 June 1967]. Hizi ni kauli za kukupa picha HAMAS wanasimamia nini na Wanapigania nini.

Radio Cairo ilitangaza kua "[Watu] Waarabu wamedhamiria kikamilifu kuifuta Israel katika ramani na kirejesha heshima ya watu wa Palestina". May 25, 1967.

May 28, 1967 rais wa Misri Gamal Abdel Nasser anasema  "Hatutakubali uwezekano wowote ule wa Israel na Palestina kuwepo pamoja".

31 May 1967 rais wa Iraq Abdel Rahman Aref anasema "Uwepo wa Israel ni dosari ambayo ni lazima irekebishwe".

Utaona msimamo mkali wa Waarabu dhidi ya Israel kwa hio salama ya Israel ilikua ni kupitia kujua namna gani atakua wa kwanza kujilinda dhidi ya maadui zake ambao wote wanatangaza kumuangamiza.

Sasa kwanini HAMAS ilianzishwa turudi 29 August 1967 kule Khartoum Sudan kulikaliwa mkutano wa Shirikisho la nchi za Kiarabu (Arab League) iliokua na makao makuu pale Cairo, Misri. Katika kilele cha mkutano huo Arab League ilikuja na azimio la HAKUNA/HAPANA TATU (THREE NOES) ikiwa ni No peace with Israel, No recognition of Israel na No negotiation with Israel [ Hakuna amani na Israel, Hakuna kuitambua Israel na Hakuna majadiliano na Israel]. Na hili linaanzia katika imani ya Waarabu hata kabla ya vita mfano tizama msimamo wa Misri na Iraq kabla ya June 5, 1967.

:::::::::::::***


Vita vya siku sita mwaka 1967 vinahitaji muda kujadili lakini matokeo kifupi vita viliisha kwa aibu kubwa mno kwa Waarabu. Lakini kwa Israeli iliwafanya wajipatie maeneo mengi zaidi kama Golan Heights kkutoka Syria, East Jerusalem kutoka Jordan, Ukingo wa Gaza na Sinai. Jumla ya maeneo haya ilikua ni mara tatu ya ukubwa wa Israel.

1973 tumeona katika sehemu ya pili kua Waarabu waliivamia tena Israel safari hii hakukua na mshindi wa wazi. Israel na Misri chini ya Marekani zikaanza mchakato wa amani. Mwaka 1978 wanakutana na kuafikiana baadhi ya mambo pale Camp David nchini Marekani.

1979 Egypt anakua taifa la kwanza la kiarabu kuvunja kiapo cha Khartoum cha mwaka 1967 na anatimuliwa kutoka Arab League na makao makuu yanagamishiwa Tunis. Kifupi ni kwamba Misri sio tu kama ilitengwa bali ilichukiwa na jumuiya nzima ya Kiarabu na zaidi Wapelestina waliona wamesalitiwa na ndugu zao. Lakini chuki ikazidi zaidi kwa Wayahudi wa Israel.

Fikiria hili.

Hadi hapo utagundua mtetezi mkubwa wa Palestina alikua ni Misri na sasa Misri kasaini makubaliano ya amani na Israel. Je, nani alibaki kuwapambania Waarabu? Ilikua hivi;

Wapiganaji wa Hamas wakiwa na silaha

KUANZISHWA KWA HAMAS

1973 Imam mmoja kutoka Palestina alianzisha "Kituo cha Kiislamu" cha kutoa misaada ya kijamii kiliitwa mujamah al-Islamiya. Kilifanya kazi kubwa kusaidia watu. Mwaka 1987 kulizuka vurugu za Wapalestina zilizofahamika kama Intifada na ndizo zilizoweka msukumo wa kubadilika kwa Islamic Centre hio (mujama al Islamiya) kua Islamic Resistance Movement. Naam HMS inazaliwa chini ya Imam Sheikh Ahmed  Ismail Hassan Yassin.

1979 Egypt anakua taifa la kwanza la kiarabu kuvunja kiapo hicho na anatimuliwa kutoka Arab League na makao makuu yanagamishiwa Tunis.

Ilikua 10 December 1987 ambapo Imam mmoja anaamua kubadili kikundi kimoja cha misaada kua kundi la kiharakati na likaitwa Harakat al Muqawamah al-Islamiyyah [HAMAS] ikiwa na maana ya Islamic Resistance Movement.  Kumbuka 8 December 1987 kuna vurugu zilianzishwa na Wapelestina wakipinga mauaji ya wapalestina wanne katika ajali ambayo wao wanadai Israel ilifanya makusudi kuwagonga hao Wapelestina kama kulipiza kisasi baada ya akari mmoja wa Israel kuawa siku takribani mbili hivi kabla ya 8 December. Hizo vurugu zinaitwa Intifada ya kwanza zilidumu kwa takribani miaka minne.

Hamas walishikilia msimamo wa azimio la Khartoum baada ya kuona kuna namna viongozi wa Palestina walikua wakiendekeza kutafuta suluhu ya amani na Israel. Kwa hio wao waliamini namna pekee ya kuelewana na Israel ni kupitia vita ambavyo wanaamini wangeshinda au watashinda.

Mfano kulikua na jitihada za kujadiliana kati ya Palestinian Liberation Organization (PLO) na Israel kule Oslo Norway. Majadiliano hayo yalifikiwa 1993 lakini hakuna hatua iliyopigwa kuyafikia.  Majadiliano haya hayakuungwa mkono na HAMAS na wakabaki kua wapinzani wakuu wa Israel. HAMAS WANATA VITA TU.

HAMAS ikapata ufadhili kutoka mataifa kama Iran na Kuwait ikasukwa kwa kuunda mkondo wa Kijeshi ambapo wana kikosi kinaitwa The Izz ad-Din al-Qassam Brigades  'Battalions of martyr Izz ad-Din al-Qassam'; au Al-Qassam Brigades chini ya mwanajihadi maarufu na pasua kichwa kwa Israel kwa sasa ambae ni Mohammed Deif. Mpaka sasa kwa taarifa za CIA World Factbook Hamas inawaoiganaji kati ya 20,000- 25,000.

Mwaka 2000 waziri mkuu wa Israel Shimon Perez alitembelea Al Aqsa sehemu  ya tatu kwa Utakatifu katika dini ya Kiislam. Wapelestina wakaanzisha vurugu ambazo zilikuja kua Intifada ya pili baada ya ile ya 1987. Sasa pia kutokana na asili ya eneo la Jerusalem pia Israel huenda imekua ikifanya machukizo dhidi ya Waislam hivyo kuundeleza uhasama baina yao.

Ukiachilia mbali kwamba wanahimiza vita dhidi ya Israel kumbuka pia wana tawi la kisiasa. Jeshi la Israel liliondoa kikamilifu vikosi vyake Gaza na kuikabidhi Gaza kwa Mamlaka za Palestina kujitawala ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya Oslo ya 1993.

Sasa Hamas walikua na nguvu upande wa Gaza na katika uchaguzi wa Palestina wa 2006 walipata kura nyingi Gaza na hivyo kuunda serikali yao mwaka 2007.  Lakini pia wana wafuasi wengi katika ukingo wa Magharibi (West Bank). Kuanzia 2007 mpka leo hakujawahi kua na mahusiano mazuri kati ya Gaza chini ya HAMAS na Israel ambayo inaitambua HAMAS kama kikundi cha Ugaidi. Kwa hio baada ya hapo Israel imekua ikihofia usalama wake hasa kutoka Gaza ambako Hamas wanatawala.

WATU TOFAUTI, ITIKADI TOFAUTI ILA LENGO MOJA.

HAMAS vs ISRAEL kitu cha kwanza kuelewa ni kwamba wote wana uchu uliopitiliza wa ARDHI. Kwa hio ni vita ya nani ana haki ya eneo ambalo sasa ni nchi ya Israel. HAMAS wanalitaka na ISRAEL wanalitaka na wamelishikilia. HAMAS hawako tayari kugawana eneo na Israel wako tayari kuongeza hata nchi moja katika ukingo wa Gaza kwa maana watafuta dhana ya Israel ya Waisrael ikibidi ila hawako tayari kupunguza hata kwa sentimita moja eneo lolote la Israel.

Suala la dini linatumika kutengeneza itikadi ya mapambano ila sio sababu ya kwanza kasoro tu linapokuja swala la Jerusalem ambapo kila mtu anautaka mji lakini ni kwa sababu za kiunabii na hofu ya labda ukweli wa kuogofya. Kwa maana Wayahudi, Wakristo na Waislamu wote wanautumia mji huo kama mji mtakatifu. Mwaka 1947 wakati wa kuigawa Palestina, Umoja wa Mataifa (UN) ulipanga utakua mji huru si Israel wala Palestina alopaswa kuudhibiti lakini kwa sasa Jerusalem yote iko chini ya Israel na ndio makao makuu mapya ya Israel tangu 2018 lakini pia Wapalestina wanataka taifa lao likiundwa basi Jerusalem uwe ndio mji mkuu wa Palestina. 

Sera za ubepari za kujitanua ni kikwazo kwa ustawi wa Wapelestina na itabakia changamoto kubwa mashariki ya kati. Makazi ya Walowezi eneo la West Bank ambako Israel imekiuka azimio la Umoja wa Mataifa la 1967 bado linawanyima usingizi Wapelestina. 

Na mwisho ni kwamba kila upande unataka kuishi. Kwa hio kama HAMAS hatopambana haki ya Palestina na watu wake inaweza kupotea kabisa sio tu kwa maana ya eneo bali watu wake, utambulisho wao na jina Palestina pia litatoweka. Na endapo Israel ikijisahau inaweza kusambaratishwa walau kwa muda. Hofu hii inafanya Israel kutumia nguvu kubwa mno kupambana. Na inateswa na unabii katika nyakati ambazo huenda ni sasa. Wanajaribu kuepuka hicho kinachosemwa kisitokee? Ikiwa ndivyo, wanaweza kupinga unabii usitimie?

Unabii na Historia vimekua vikifanya mzozo huu kutokua na suluhisho kamilifu na thabiti na la mapema. Kwa Israel ni nchi ya ahadi kutoka kwa Mungu na kwa Palestina ni nchi waliyorithishwa vizazi na vizazi. Na vita hivi vitakuepo kwa muda mrefu. Sio vya kwanza na haviwezi kua vya mwisho. 

 

                                       Gaza

Kwani wana hakika kwamba Israel iliyosemwa ni hii ya kwao?

Tuchambue nini tena?

Kwa maoni, ushauri, maswali na majibu mengine zaidi unaweza kuwasiliana nami kupitia njia zifuatazo.

Email: karlrck@gmail.com

Phone: 0787505800

No comments:

Post a Comment