Wednesday, 10 August 2016
MASOMO YA SAYANSI NI LAZIMA KWA WANAFUNZI WOTE.
Waziri wa Elimu, Teknolojia, Sayansi na Mafunzo ya ufundi Prof. Joyce Ndalichako.
SERIKALI imetangaza mwongozo mpya kuwa kuanzia sasa masomo ya sayansi ni lazima kusomwa na wanafunzi wote wanaosoma elimu ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne. Kwa mujibu wa Sera ya Elimu iliyopo, wanafunzi wanaosoma elimu ya sekondari wanaweza kuchagua aina ya masomo watakayo wafikapo kidato cha tatu na kuacha mengine.
Uamuzi huo ulitangazwa jana mjini hapa na Waziri wa Elimu, Teknolojia, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako wakati akizungumza na mamia ya walimu wa elimu ya msingi kwenye mafunzo ya muda mfupi kuhusu mtaala mpya wa kufundishia wanafunzi wa darasa la tatu na nne.
Alisema hivi sasa nchi imedhamiria kuingia kwenye uchumi wa kati ambao ni wa viwanda, hivyo suala la sayansi haliwezi kuepukwa kwa sababu ni wakati sasa wa kuwa na wataalamu wengi wa fani za sayansi watakaoweza kutosheleza mahitaji ya sekta ya viwanda nchini.
Alisema kutokana na uhaba wa wataalamu wa sayansi nchini kwenye maeneo mengi, wizara imeamua kuanzia sasa wanafunzi wote wa elimu ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, watalazimika kusoma masomo ya sayansi na kufanya mtihani wa masomo hayo, na kwamba baada ya matokeo kutoka ndipo watafanya uamuzi ama wa kuendelea nayo au la.
Hatua hii kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, itamlazimisha mwanafunzi kusoma kwa bidii ili kuhakikisha anafaulu masomo hayo ingawa hivi sasa wanafunzi walio wengi wanadai masomo hayo ni magumu, ndiyo maana wanachagua kusoma masomo ya sanaa.
Alisema ili kuhakikisha azma ya serikali ya wanafunzi wanapata vitendea kazi vya masomo hayo, Sh bilioni 12 zimetengwa kwenye bajeti ya fedha ya mwaka huu kwa ajili ya kununulia vifaa vya maabara kwenye shule zote za sekondari nchini ili kuwepo na zana za kufundishia kwa ajili ya masomo ya sayansi.
"Mafunzo ya vitendo sasa sio mbadala ni lazima, na yatafanywa kama sehemu ya masomo na wanafunzi wote watalazimika kuyafanya kwa vitendo ili wawe na uelewa wa walichosoma kwa manufaa ya taifa,” alisema Profesa Ndalichako.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment