Tuesday, 26 July 2016

HUKUMU ILIYOTOLEWA NA MAHAKAMA KUU JUU YA KESI YA DAUDI MWANGOSI.

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Iringa imemtia hatiani askari Polisi Pacificius Cleophace Simoni kwa kosa la mauaji ya bila kukusudia ya mwanahabari Daudi Mwangosi yaliyotokea Septemba 2, 2012 katika kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi mkoani Iringa.

Kwa mara ya kwanza Simoni alifikishwa mahakamani hapo Septemba 12, 2012 akituhumiwa kufanya kwa kukusudia mauaji hayo wakati mwandishi huyo alipokuwa akiwajibika katika kazi zake za kutafuta habari kwenye ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Ushahidi usiojitosheleza uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa Jamuhuri umeilazimisha mahakama hiyo chini ya Jaji huyo kuibadili kesi hiyo kutoka kwenye mauaji ya kukusudia na kuwa ya mauaji ya bila kukusudia ambayo hukumu yake ameisogeza mbele hadi Jumatano, Julai 27.
Baada ya mabadiliko hayo, wakili wa upande wa Jamuhuri Adolph Maganga aliiomba mahakama hiyo imuhukumu mtuhumiwa huyo kifungo cha maisha jela kwa mujibu kifungu cha 198 cha sheria ya kanuni ya adhabu huku wakili wa utetezi, Lwezaula Kaijage akiiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu mtuhumiwa huyo kwa kumfunga kifungo cha nje.
Akiiomba mahakama itoea adhabu ndogo ya kifungo cha nje kwa mtuhumiwa huyo, Lwezaula aliiomba mahakama hiyo imuonee huruma mtuhumiwa huyo kwakosa alilofanya bila kukusudia kwasababu ni kijana mdogo mwenye miaka 27 anayetegemewa na Taifa kama nguvu kazi.
“Na alishiriki oparesheni iliyosababisha maafa hayo bila ridhaa yake, amekaa mahabusu kwa miaka minne na katika kipindi hicho atakuwa amejutia sana kosa lake, amefiwa na wazazi wake wote wawili, ana wadogo zake watano wanaomtegemea na ana mke na mtoto mdogo mmoja,” alisema wakili huyo wakati akitoa ombi hilo.
Kwa msingi huo, wakili huyo alitumia kifungu cha 38(11) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kuomba mahakama imuhurumie mtuhumiwa huyo na kumfunga kifungo cha nje.
Akisoma maelezo ya kesi hiyo kabla ya kuibadili na kuwa na mauaji ya bila kukusudia, Jaji Kiwehlo alisema upande wa Jamuhuri uliletea mashahidi wanne ambao kati yao watatu walitoa ushahidi ulioshindwa kuithibitishia moja kwa moja mahakama kama mtuhumiwa huyo alikusudia alipofanya mauaji hayo.
Huku akishangaa kwanini Jamuhuri pamoja na kuwa na rasilimali za kutosha ilishindwa kuwaleta mashahidi wengine muhimu kama Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa wa wakati huo, Michaela Kamuhanda na Afisa Upelelezi wa Mkoa Wankyo, aliwataja mashahidi hao kuwa ni Said Mnuka, Azel Mwampamba na Lewis Obado ambao pi awote walikuwa askari Polisi wa vyeo tofauti.
Alisema ushahidi pekee uliomtia hatiani mtuhumiwa huyo ni ushahidi uliotolewa na shahidi namba tatu ambaye ni mlinzi wa amani Frola Mhelela.
Mlinzi huyo wa amani aliwasislisha mahakamani hapo ungamo la mtuhumiwa huyo lililomuhusisha na mauaji hayo na ambalo wakati likiwasilishwa upande wa utetezi haukulikana pamoja na kwamba ulikuja kulikana baada ya ungamo hilo kuwasilishwa mahakamani hapo.
Kwa kupitia ungamo hilo ambalo mahakama imejiridhisha bila shaka yoyote kwamba maelezo yake yalitolewa kwa hiari na mtuhumiwa huyo; mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na mauaji hayo japokuwa alisema yalikuwa ni ya bahati mbaya.










No comments:

Post a Comment