Friday, 22 July 2016
MAALIM SEIF KUTINGA MAHAKAMA YA ICC
Wakati polisi wakisema wanasubiri jalada la Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad litoke kwa Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) ili wamfikishe mahakamani kwa uchochezi, leo atakwenda katika Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC) kuwashtaki viongozi wa Serikali.
Maalim Seif anakwenda kuwashtaki viongozi hao kwa madai kuwa, walitumia mamlaka yao vibaya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kisha kuwatesa, kuwakamata na kuwapiga wafuasi wa chama hicho bila makosa.
Mei 22 mwaka huu, chama hicho kilizindua ripoti yake ya uvunjwaji haki za binadamu Zanzibar wakati wa uchaguzi huo na kutangaza azma yake ya kwenda ICC kuwashtaki Waziri wa Mambo ya Ndani na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP).
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema jana kuwa mpango huo umekamilika na Maalim Seif ambaye yupo nje ya nchi kwa ziara ya kueleza alichodai ‘figisufigisu’ zilizotokea katika uchaguzi mkuu, ataweka wazi kila kitu kilichotokea na jinsi ukiukwaji demokrasia ulivyoshika kasi nchini.
Source.Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment