TRUMP NA MAREKANI VS NICOLAS MADURO NA VENEZUELA, JE, VITA IKO KARIBU?
![]() |
| Rais wa Venezuela Nicholas Maduro. Picha na Reuters |
Kumekuwapo na sintofahamu kubwa juu ya kile kinachoendelea kati ya Marekani na Venezuela kufuatia matendo hatarishi ya pande zote mbili. Awali Marekani ilitangaza dau nono la dola milioni 50 ambazo ni sawa na karibu sawa na shilingi 12, 529, 390, 000/= kama zawadi kwa mtu yeyote anatakaye wezesha kupatikana na kukamatwa kwa Rais wa Venezuela ambae anatuhumiwa kwa ulanguzi wa madawa ya kuelevya. Lakini hilo limechukua sura mpya baada ya Marekani kutuma meli za kivita pamoja na nyambizi karibu na Venezuela kitu ambacho kimemlazimu Rais Maduro kuanza kukusanya wanajeshi wakijiandaa kwa makabiliano ikiwa Marekani itawavamia.
Katika kile kinachoonekana kama ni ujumbe wa rais Maduro kwa Marekani alionekana kukerwa na taarifa za uwepo wa meli kadhaa za kivita katika pwani ya Karibeani kusini karibu na nchi yake na alisikika akisema ikiwa Marekani itafanya uvamizi nchini Venezuela basi wajue hawatashinda. Hawajahi kushinda na hawatokuja kushinda kamwe na kiwataka wafuasi wake kupambana dhidi ya uvamizi wa kigeni. Licha ya kwamba ni kawaida kwa jeshi la Wanamaji wa Marekani kufanya doria katika eneo la Karibeani kusini, hii ya sasa imepitiliza kile ambacho hua kinafahamika kwamba kipo.
Kuna taarifa kua Rais Donald Trump ameagiza kupelekwa kwa meli za kivita zaidi ya saba na nyambizi moja ya mashambulizi inayoendeshwa kwa nguvu ya nyuklia. Hili limekua sio kawaida sana. Ijapokua Trump amekua akikabiliana vikali na magenge ya walanguzi wa dawa za kulevya katika eneo la Amerika ya Kati lakini hatua hizi zinaonekana kua za juu zaidi. Kulingana na taarifa mbalimbali zilizopo ni kua miongoni mwa meli zilizoko au zinazoelekea karibu na Venezuela ni pamoja na USS San Antonio, USS Iwo Jima na USS Fort Lauderdale zikiwa na jumla ya wahudumu 4500 ambapo 2,200 kati yao wakiwa ni wanajeshi wa jeshi la Marekani.
Kufuatia hatua hiyo Rais wa Venezuela Nicholas Maduro ameilaumu Marekani kwa kufuata kile alichokiita diplomasia ya vitisho iliyokuepo miaka 100 iliyopita. Na akatangaza kuandikiaha wanajeshi au wanamgambo wapya na kufanya mazoezi kila siku ya Ijumaa na Jumamosi. Hatua kama hizi zinaweza kuchochea zaidi mvutano na baadaye kuingia katika vita. Ikumbukwe kwamba Rais Nicholas Maduro anaitazama Marekani kama adui na amekua akiishutumu Washington kutumia vikosi vya CIA kushirikiana na wanasiasa wa upunzina wa Venezuela kuhakikisha anatoka madarakani. Wakati huo huo Marekani inamchukulia Maduro kama kiongozi wa genge kubwa la kilalifu na ulanguzi wa madawa ya kulevya na sio kiongozi halali wa Venezuela.
Katika mitazamo hiyo kunaweza kuibuka kisingizio cha vita. Wizara ya ulinzi ya Marekani mpka naandika katika blog hii ilikua bado haijatoa taarifa rasmi ya kile kinachoendelea Karibeani ya Kusini huku ikulu ya Marekani ikisema kua Rais Trump alikua tayari kutumia mbinu au njia yeyote yote kupambana na ulanguzi wa madawa ya kulevya na uhamiaji haramu. Ni nini kitajiri kati ya Marekani na Venezuela ni swala la kusubiri na kuona.

Comments
Post a Comment