DUNIA INAHAMIA WASHINGTON KWA MUDA: WASHINGTON NI YA MOTO
DUNIA INAHAMIA WASHINGTON KWA MUDA: WASHINGTON NI YA MOTO
Rais wa Ukraine kushoto akifurahia na mwenyeji wake Rais Donald Trump wa Marekani, ikulu ya White House Agosti 18, 2025. Picha na Reuters
Leo jijini Washington inatazamiwa kua ni moja kati ya nyakati ngumu na muhimu zaidi tangu vita vya Pili vya dunia vilivyomalizika mwaka 1945. Wakati kulishuhudiwa nyakati ambapo viongozi wengi wa dunia wapishana katika makao makuu ya nchi kama kubwa au miji iliyokua na ushawishi kama vile Potsdam huko Ujerumani na Yalta huko Crimea nchini Urusi.
Baadae Washington ikawa kitovu cha mikutano mikubwa ya kuamua hatma ya siasa na maendeleo ya dunia kwa kua miji ya Ulaya kama vile Berlin, Brussels, Vienna na London ilikua imepoteza ushawishi wake. Na Washington imebakia kama kielelezo cha Ushawishi duniani ambapo viongozi mbalimbali hukutana.
Leo Agosti 18, tayari Washington imepokea viongozi wa Ulaya wakiongozwa na rais ya kamisheni ya Umoja wa Ulaya bi. Ursula von Layen, Waziri mkuu wa Italia bi. Giorgina Meloni, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Waziri mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz na rais wa Ukraine Volodymr Zelenisky wanaotarajiwa kufanya mazungumzo na rais wa Marekani Donald Trump kuhusu kusitishwa kwa vita huko Ukraine. Lakini viongozi wote wameambatana hapo wana hofu kubwa kila mmoja akihofia kesho yake dhini ya kitisho kimoja angalau kwa sasa; rais wa Urusi Vladimir Putin. Naam, ndiye kiongozi ambaye anaogopwa sana huko Ulaya kwani anaweza kua hamalizani tu na Ukraine, huenda akawa na mpango mwingine wa kuudhoofisha Umoja wa Ulaya na NATO. Hili linaleta hofu kubwa sana.
Viongozi wa Ulaya wanataka amani ambapo haitahisishwa Ukraine kupoteza ardhi yake kwa Urusi kwani mipika ya Ulaya itakua lazima kuchorwa upya. Hii ni historia ya Ulaya mipaka yake hubadilika badilika sana lakini kwa kipindi kama hiki inabadilika kwa njia ya ubabe mwingi na mabavu sio makubaliano kwa hio Ukraine kupoteza sehemu ya ardhi ni kwamba Umoja wa Ulaya umepoteza kwa Putin na Urusi kwa mara nyingine tena. Kwani kufanya hivi kunaweza kumpatia Putin au kiongozi mwingine motisha na hamasa ya kujitwalia maeneo ya nchi nyingine kinguvu.
Hio ndio sababu kubwa viongozi wakuu wa Ulaya wameelekea Washington DC. Wanataka kutumia sauti ya pamoja kuomba na kumsukuma Trump kuwaamini wao na sio rais Putin. Wanataka kumsukuma kuibinya Urusi na Putin kukubali pendekezo za amani na sio kuibinya Ukraine. Kwa sababu baada ya kutoka Alaska Donald Trump alisema Ukraine inapaswa kufanya amani na Urusi kwa kua Urusi ni taifa lenye nguvu sana na Ukraine hawana nguvu. Matamshi hayo yanaonesha Trump yuko "desperate" (yaani amejichokea anachotaka ni amani tu) na hajali nani atapoteza nini. Kwa sababu ikiwa amani itapatikana, Trump anajitangaza kua "Mfalme wa amani". Na hili ndilo analitaka. Na viongozi wa Ulaya wanaogopa hali hio ya Trump kwani Ukraine anaweza kuonewa ili kukidhi haja za viongozi wawili wenye shauku na ndoto kubwa ilihali shauku na ndoto zao ni tofauti.
Rais wa Ukraine kushoto pamoja na Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Layen walipokua katika mkutano wa pamoja huko Brussels kabla ya kuondoka kwenda Washington DC, Marekani mwezi Agosti, 2025. Picha na AFP
Kwa upande wa Ukraine hata jana huko Brussels, rais wa Ukraine alisema swala la kubadilishana maeneo litahitaji mjadala wa pande tatu na litajadiliwa baina ya Urusi na Ukraine pekee. Katika matamshi yake utagundua anahofu kubwa kwamba huenda Uktaine ikalazimika kuachia eneo la Crimea lilotwaliwa mwaka 2014 na eneo la Donbas linalojumuisha maeneo kama vile Donetsk na Luhansk. Eneo lote la Ukraine linalokalisa kimabavu na Urusi ni takribani 19% ya ardhi yote ya Ukraine. Kitu kigumu ni kwamba watu wengi na wanajeshi wengi wa Ukrane wamekufa kutetea ardhi yao, leo inakuaje ardhi waliojitolea kuilinda kwa damu inaenda kwa adui? Je, ni bora kuendelea kupambana au wakubaliane na matakwa ya Trump na Putin?
Jana Jumapili Rais Trump alisema kupitia mtandao wake wa Truth kua Zelenisky anaweza kumaliza vita haraka iwezekanavyo au anaweza kuendelea kupigana. Na alisema kua Ukraine ilikua imeiachia Crimea kipindi cha Obama miaka 12 iliyopita bila kumwaga damu na sasa wanaweza kufanya hivyo. Akimaanisha kuachia baadhi ya maeneo ya Ukraine na kutangaza kua Ukraine haitojiunga na NATO kamwe! Ambapo alifokeza kua mambo mengine yatabakia hivyo hivyo bila kubadilika. Akimaanisha swala la Ukraine kutojiunga NATO halitabadilika. Mara baada ya kauli hio Ulaya yakatoka majibu kwa Zelenisky kua ilikua ni makosa kuiachia Crimea kipindi hicho kwa sababu imetumika kama kituo cha uvamizi wa mwaka 2022. Na kua kwa sasa hawatoachia eneo la kimkakati la Donbas. Ijapokua juu ya ulinzi wa Ukraine, inasemekana rais Putin aliiubali kutolewa kwa garantii ya kiusalama kwa Ukraine inayofanana na ile ya kifungu cha 5 cha mkataba wa wanachama wa NATO.
Endapo Rais Zelenisky na viongozi wa Ulaya watasema hilo haliwezi kutokea au kuwezekana kabisa kuna hatari Marekani akaaha kutoa msaada nchini Ukraine na akaanza kuilaumu Kyiv kwa kushindwa kufikia makubaliano ya kumaliza vita. Na bila msaada wa Marekani huko Ukraine nahofia kusema Ulaya pekee haiwezi kuilinda Ukraine kwa hio itakua ni swala la muda kabla ya Ukraine yote kukaliwa na au kutwaliwa na Urusi. Hili nalo kila mtu hataki litokee.
Wakati huo huo rais wa Marekani Donald Trump atatamani kuona vita inaisha ili abaki ile hulka yake anayoitaka ya mleta amani na pengine aje kushinda Tuzo ya Amani ya Nobel (Nobel Peace Prize). Lakini anajua kikwazo kikubwa ni Putin. Kwa sanabu anaweza kuzitishia nchi za Ulaya magharibi kwa namna nyingi lakini hawezi kuishia Urusi kwa namna hio hio zaidi ya vikwazo vya kiuchumi kwa Urusi na washirika wake. Lakini njia zote ni hatari. Urusi yenye uchumi mkubwa na imara itakua kitisho kwa Ulaya na Urusi yenye maumivu kiuchumi na kidiplomasia itakua hatari zaidi. Kwa hio hapa pia, Trump atahitaji busara sana ili baadae Marekani isijekua na maadui wawili wenye nguvu karibu sawa na yake; kwa maana ya Urusi na China.
Putin atakua zake Kremlin huko anafanya mazoezi, anatembea na mbwa wake anakula na kunywa kuona ni nani kati ya wale walioko Washington amekua wa kwanza kuingia katika mtego wake. Huyo ndio "master minder" wa huu mchezo. Amewagawa sana na kufanya makubaliano kuaagumu. Kadri watakavyochelewa kupata suluhu ndivyo atavyoendelea kujitwalia ardhi huko Ukraine.
Imeandikwa na;
Erick Jerry
karlrck@gmail.com


Comments
Post a Comment